Nchi yangu+Njaa yangu+Tamaa yangu

Kwanza Namshukuru Baba Mungu anaye nijalia uzima na rehema tele na hata kuniwezesha tena kuandika hii makala.Pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa mhariri wa gazeti hili kwa kukubali kutoa makala yangu ili iweze kusomwa na jamii yote ya watanzania watakao bahatika kulisoma hili gazeti.
Kwa kifupi mimi ni mchagga kutoka machame Jimbo la Hai Mbunge wangu ni Freeman Mbowe japo mwaka huu amekataa kugombea tena natamani angebadili uhamuzi. Ni msomi wa shahada ya kwanza ya Electroniki na Mawasiliano kutoka katika chuo kikuu cha Dar es salaam sehemu ya mlimani.
Nimekuwa katika ajira kwa muda wa miaka mitano sasa na nimekuwa nikifanya kazi sehemu tofauti tofauti sana kwa muda wote wa miaka mitano.Nimefanya kazi serikalini,nimefanya kazi na wahindi,nimefanya kazi na wazungu pia nimefanya kazi na waarabu.
Unaweza kuona miaka mitano ni michache sana niliwezaje kufanya kazi na hao watu lakini kuna sehemu nimeshawai kufanya kazi nusu mwezi.Hii yote ni katika ule msemo usemao kuishi kwingi ni kuona mengi.
Nimeshuhudia mambo mengi sana katika ajira hizi hasa ajira za makampuni binafsi na wawekezaji.Ni vigumu kumwambia mtu ambaye hajawai kufanya kazi akuelewe maana kinachosemwa na kilichopo huko ni tofauti kabisa.
Hawa watu wanaitwa wawekezaji wananyanyasa sana watanzania masikini.Watu wanapata sana shida huko makazini hakuna sehemu ya kupeleka kilio chao maana kila eneo limezibwa na zege nzito hakuna upenyo wa kupitisha vilio vyetu ukapata nafuu.
Hawa wawekezaji tunawakaribisha kwa masharti nafuu sana tunawapa maeneo mazuri ya kibiashara na wanapata pesa tena nyingi kutoka kwetu lakini hawa watu ni wabaya sana kwetu.Pesa ndio silaha yao kubwa ya kujilinda na kutumaliza sisi washika dau.
Ukweli kabisa ajira Tanzania kwa sasa ni ngumu ukiacha kazi mpaka uje upate tena ajira nyingine ni zaidi ya mwaka na kama hauna refa ndio kabisa umekwisha.
Unapokuwa na ajira inabidi uilinde kwa namna iwayo yote ili uhakikishe haikuponyoki.
Sasa hapo ndio matatizo na mateso yanapokuja maana unajitahidi uilinde ajira yako na hawa watu pia wameshajua kuwa Tanzania kuna tatizo la ajira wakikupa kazi ukubali kuwa mtumwa na si mfanyakazi.
Watu wanabaguliwa makazini jamani watu wanatengwa tena wazi wazi kabisa sababu tu hii ya ngozi au umaskini au elimu au ni afrika ni nini?.
Umesoma lakini inafikia mahali unaona hata elimu yako si chochote sababu ya kunyanyaswa kwenye ajira.Watu wanatukanwa wanadharauliwa wanatishiwa kufukuzwa kazi na ikibidi wanakufukuza kama mbwa tena bila malipo na huna pa kwenda.
Utaenda wapi wakati walafi wote wa serikalini wanaohusika na kukutetea wewe wanapokea kifunga mdomo kila mwisho wa mwezi kama asante,wahariri walafi wanapokea mishahara kila mwezi kwa kuchana na kutupa malalamiko ya watu wanayoletewa na mbaya zaidi wanakwenda kuwaripoti wale wote wanaowaletea habari mbaya za kampuni ya bwana mkubwa ili wafukuzwe kazi,Ukienda polisi unajikuta wewe ndio unawekwa ndani binafsi ilishawahi kunitokea nilifukuzwa kazi sehemu fulani nikanyanganywa na computer yangu binafsi nilikuwa naitumia ofisini kwangu nikaenda kuripoti polisi lakini nikajikuta mimi ndio nawekwa ndani na mshtakiwa wangu anadunda nje.
Ukienda Labour kwenye haki za wafanyakazi kuna walafi huko wanapokea hela kila mwezi kutoka kwa mabwana wakubwa ili kesi zao zikifika huko wazirefushe na baadaye wazifute nendeni kule labour mkaone nazungumza kwa ushahidi nimekuwa pale kwa shida zangu bila msaada.Utafuatilia madai yako miaka na miaka utapigwa tarehe mpaka utachoka. Ulikuwa unadai milioni mbili utapewa laki moja kama hutaki hupewi kabisa.
Kwenye mambo ya jinsia ndio tena usiseme,bora tena kidogo na wanaume wanawake maskini ndio kabisa haifai hata kuelezea kama nasema uongo fatilieni mtaona.Mabinti zetu hawa wanafanyishwa ngono chafu tena za lazima bila hiari sababu ya ajira.
Waulizeni watawambia wamesota miaka mingapi kupata kazi leo hii ameipata kazi anaogopa kuacha. Hawa maboss wanawatisha ili wawape ngono tena ngono chafu kabisa.
Hawa wanawake wanalazimika kukukubali ili wapate ajira wakijua itakuwa mara moja badala yake inakuwa ni kila siku anakuwa mtumwa wa ngono kwa kuwa alianza taratibu inafikia mahali anazoeshwa hiyo tabia tayari anakuwa ameshaharibikiwa na hii mpaka kwa wake za watu.
Najua hii tabia ipo sehemu nyingi lakini ukweli kabisa mfano serikalini kidogo kuna uwazi unaweza hata kusema lakini kwa hawa watu utasema wapi maana kwa kufukuzwa kazi ni nje nje na maisha ni magumu watu wanaogopa. Wanawafanya vibaya wakishawaharibu wanawafukuza kazi ni mateso makubwa ndani ya nchi yetu. Tena na sehemu zingine wanawake hawaruhusiwi kushika mimba wakishika tu mimba kazi hakuna.
Saa zingine mimi nawashangaa hawa wanajiita wanatetea haki za binadamu haki za wanawake kivipi hizo haki mnatetea namna gani watu wanapata mateso makubwa namna hii mkiwa wapi au mnafanya kazi kwa utaratibu gani zaidi ya kukaa kwenye meza nzuri zilizotandikwa na vitambaa laini na kukalia masofa ya gharama huku mkinywa na kula pesa za wafadhili ambao mmewadanganya mnazitumia kutetea maslahi ya watu, Ole wenu.
Suala jingine kwa hawa wawekezaji ni tofauti ya mishahara kati ya wafanyakazi wanaowatoa kwao na wafanyakazi wa hapa nchini.Kwa mfano mimi nina shahada ya kwanza na vyeti vingine vya kozi fupi fupi lukuki ukichanganya na uzoefu nilio nao kimsingi napaswa nilipwe mshahara mkubwa kama wao katika kampuni yetu lakini utashangaa mtu kama mimi na pengine nimemzidi hata uzoefu hata mwaka wa kumaliza chuo nimemzidi lakini kwa kuwa tu katoka nje ya nchi wamemleta wao wanamlipa mshahara mkubwa tofauti na mimi.
Sasa kama mimi mfano, nalipwa laki mbili na nusu na wao wanalipwa milioni nne na nusu tena wanapewa nyumba maeneo ya masaki,msasani,mikocheni au oysterbay na gari nzuri ya kutembelea,wanajaziwa mafuta pia wanawasomeshea watoto shule za kimataifa, kuna usawa gani hapo?.
Mimi nikichukua lakini mbili na nusu yangu tena ni gross inabidi ikatwe kodi na NSSF sana sana nakuja kubakiwa na kama laki hivi na omba Mungu usikute ulichukua mkopo,elimu tuko nao sawa kazi tunafanya sawa tatizo ni nini?sijui.
Binafsi sijui kuna chombo gani kinatumika kufuatilia hawa watu baada ya kupewa mikataba na udhamini wa kufanya kazi nchini au sijui ni masharti gani wanakuwa wanapewa kuhakikisha kuwa wanaishi na kufanya kazi nchini kikamilifu kabisa ndani ya hayo masharti.
Kuna haja kubwa ya serikali kusikiliza haya mambo na kuyafanyia kazi na ikiwezekana kuwafatilia hawa watu kwa ukaribu kabisa kama ni vyama vya wafanyakazi basi viundwe sehemu za kazi na viwe huru kabisa kabisa kisheria kuweza kuwasaidia wafanyakazi. Pia serikali iwape masharti makali ya ajira na sera za kazi ziwe kwa watu wote ikibidi basi kiwepo chombo maalumu ambacho kitakuwa kinafuatilia utendaji kazi wa wawekezaji wote na pengine kukaa na wafanyakazi kwa uhuru kabisa na kusikiliza malalamiko yao.
Kumekuwa na tabia mbaya ambayo inafanywa na hawa wawekezaji siku ambayo wanajua anakuja kiongozi mkubwa serikalini watahakikisha hampewi nafasi hata kidogo ya kutoa shida zenu na pia siku hiyo watajidai kusoma risala nzuri sana kuhusu utendaji kazi wao na jinsi wanavyowajali.Viongozi nao mara nyingi wanakuwa wanaamini hayo na wanaondoka huku wamefungiwa mazawadi kibao kwenye magari yao.
Shida zinabaki huku nyuma kama zamani tupeleke wapi kilio chetu.Ni nani kiongozi mwadilifu kabisa kabisa anayeweza kuja awaulize watu shida zao na awasaidie akatae zawadi na aseme ziiuzwe na hizo fedha watu waongezewe katika mishahara yao.
Tunajivunia kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na kuwa moja ya nchi zinazopata wawekezaji wengi lakini je haya madhara yanayoletwa na wawekezaji ni nani anajitolea kuyashughulikia na kujisifu ameweza kupambana nayo.Je ni sawa kwamba nchi inapata wafanya biashara wengi wa nje lakini wananchi wake tunayanyaswa na kudhauriwa,wanawatumia dada zetu kwa ajira za ngono kama wapendavyo tena kwa kujisifia.Hebu jaribu kwenda kuwekeza kwao halafu fanya ushenzi kama huu uone kama watakuacha.
Heshima ya nchi kama nchi iko wapi? kwa nini tusisimame na umaskini wetu tukasema NO! HAPANA! tupewe heshima,tutambulike na tukubalike. Tuna akili na tunaweza kwanini kama kuna wachache wetu wanatuuza tusiwachome moto wapotee juu ya uso wa nchi, mfano kumbuka filamu ya SARAFINA walimchoma moto Sabela maana alikuwa anatumiwa na makaburu kuwadhalilisha na kuwatesa weusi wenzie.
Nina imani serikali imeweka mpango wa kuruhusu wawekezaji waje nchini kwa nia nzuri kabisa na haya tunaweza kusema ni matokeo ya uwekezaji ok! sasa tufanyeje? Kwanza tusiwape nafasi ya kuona kuwa wanaweza kutugawa sababu ya pesa,tusiwape nafasi ya kutudharau na kutudhalilisha na asiwepo kati yetu wa kukubali kupokea pesa ili auze utu wetu aiuze damu yetu wote tuwe kitu kimoja na tuonyeshe ushirikiano.
Wasi wasi wangu mkubwa ni kuwa leo wanacheka na viongozi hawa kwa kuwa ndio wamewapa mikataba sisi tuna wafanyia kazi wanatudharau kabisa kesho hao viongozi watastaafu itakuwaje.
Je hatuoni kama tunaachia nchi taratibu kwa sababu ya njaa zetu za msimu sababu ya ulafi wetu!, kama unamruhusu akupe pesa wewe ili anidhulumu haki yangu kesho unajua atakupa nini ili aidhulumu nchi yako...?
Natamani hizo zama zisije zikanikuta maana sitakuwa na machozi ya kulia na ni heri ukoloni wa mababu zetu kuliko huo ujao.
Watu wanaona lakini hakuna mtu anayeelewa, maana watu wanaona kwa pamoja lakini mtu anaelewa mmoja mmoja.
Tulisema Elimu ndio hazina ya watoto wetu lakini hata elimu yako inakuja kudharauliwa sababu umetoka Afrika. Je ambao hawakusoma kabisa watakuwaje? Ilihali sisi tuna elimu tunaonekana nyanya.
Hii hazina wazazi wetu wanayotupa tuifanyie nini sasa. Tuanitajika kusimamisha kwanza Utu wetu na heshima ya taifa letu ndio mambo mengine yafuate.
Hatuwezi ndio kuukwepa utandawazi lakini pia lazima tusimamishe heshima ya nchi na wananchi wake tuache tamaa za fisi tuwe na ubinadamu tudhaminiane na kuujali umuhimu wa mtu.
Na ukijaribu kuangalia haya mambo utagundua kuwa na sisi wenyewe tunachangia, maana wapo wachache wetu wanalaghaiwa ili watugeuke na kukosa msimamo.Tupambane na ubaguzi wowote ule kwa pamoja na tupambane na umaskini wa taifa kwa pamoja na sio kuweka tamaa mbele na njaa njaa za kilafi zisizo na staha.
Nina imani kama hayo yakifanyika kwa uhaminifu kabisa kabisa basi hatutadharauliwa tena wala kutengwa tutafurahia wawekezaji wetu.Kwa manufaa ya nchi yetu na heshima ya taifa letu.
Mungu ibariki Afrika,Mungu ibariki Tanzania.
Naitwa Terrie Swai ni Ni Mtaalamu wa mambo ya Computer na Mawasiliano-Dar es salaam.
+255 744 462 089
terrie.swai@gmail.com

2 Comments:
Wallahi, haya mambo yanauma sana. Tufanyeje? Mbona shida shida kote kote - ukienda kwenye nchi za hao wawekezaji napo pia makazini ukiwa na hii jezi nyeusi inabidi ufanye kazi bila dosari ili usinyanyaswe, dosari kidogo.. basi utatetwa mpaka upaone pachungu, japo una shahada zaidi ya bosi wako...
Tutasawazisha. A luta continua
Duuh, Bw Swai! Kwa kweli inatia uchungu sana. Pole sana papangu! Sasa Bongo wanyonge wafanye nini ili wapate haki kwenye hali kama hiyo kila mtu ambapo kila mtu ana njaa na tamaa?
Post a Comment
<< Home