Monday, August 15, 2005

Nyama ya sungura yamtoa roho


Mtu mmoja amekufa baada ya kujirusha kutoka ndani ya gari alilokuwa amepanda kutaka kuwahi kitoweo cha sungura aliyegongwa na gari hilo. Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Bw Abdalah Mssika, alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Nhegezi, wilayani hapa.

Kamanda Mssika alimtaja marehemu huyo kuwa ni Kisabo Kamata (35). Alifafanua kuwa, marehemu alikuwa ni kibarua wa kupakia mchanga katika gari lenye namba za usajili T. 298 AEA Isuzu Tipper lililokuwa likiendeshwa na Amour Said (35).

Kamanda Mssika alisema gari hilo likiwa njiani kurudi mjini na vibarua saba wa kusomba mchanga, liligonga sungura. Alisema baada ya vibarua hao kumuona sungura huyo, walimpigia dereva kelele kumutaka asimamishe gari ili wachukue kitoweo hicho.

Hata hivyo, kabla gari hilo halijasimama vizuri, ndipo marehemu aliporuka na kuangukia mgongo kitemdo kilichomfanya avunjike uti wa mgongo. Kamanda Mssika alisema mtu huyo alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa lakini alifariki dunia baadaye.

Katika tukio lingine, mwendesha pikipiki amekufa papo hapo baada ya kugonga ng’ombe aliyekuwa akikatisha barabarani. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki eneo la Bijampora, wilayani Kahama. Kamanda Mssika alimtaja marehemu huyo kuwa ni Dominick Gachunda (45) ambaye alikuwa akiendesha pikipiki yenye namba za usajili SH 1043 aina ya Yamaha.

Alisema baada ya kumgonga ng’ombe huyo, alianguka chini na kupoteza fahamu mpaka alipookotwa na wasamaria wema na kukimbizwa hospitalini. Hata hivyo, alisema baada ya kufikishwa hospitalini na kuchunguzwa ilibainika amefariki dunia.

Kamanda Mssika alisema baada ya mtu aliyekuwa akiwachunga ng’ombe hao kuona tukio hilo, aliwaswaga ng’ombe wake na kukimbia na kwamba juhudi za kumtafuta zinaendelea ili afikishwe mahamakani kujibu shtaka la kuacha ng’ombe katika barabara ya magari na kusababisha kifo.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home

WAGONJWA WA KANSA
WAGONJWA WA KANSA
Niandikie