Monday, November 14, 2005

Mzazi kafiri

Mtoto mdogo wa kike ambaye ni hivi karibuni ametimiza miaka tisa, Thecla Nyangige, 9, amelazwa akiwa hoi kwenye wodi mojawapo ya hospitali teule ya Nyerere wilayani hapa kufuatia kipigo kikali anachodaiwa kupewa na mama yake mzazi kabla ya kumwagiwa ’mimaji’ ya moto na mlezi wake huyo aliyemleta duniani. Kinachosikitisha na kuwashangaza wengi wanaofika kumtazama kwa uchungu mtoto huyo hospitalini Nyerere, ni sababu ya kufanyika kwa unyama huo na MAMA MZAZI wa kabinti hako ambayo yenyewe inaelezwa kuwa eti, ni adhabu kwa mtoto anayedaiwa kutenda UOVU wa KUTOOSHA VYOMBO vya chakula nyumbani kwao! Tukio hilo la kusikitisha limetokea tarehe Oktoba 15 mwaka huu na linadaiwa kufanywa na mama mzazi huyo aitwaye Laurencia Shija, mwalimu katika shule ya msingi Kisangura wilayani hapa. Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini alikolazwa, mtoto Nyangige amesema alipigwa na mama yake aliye ’ticha’ baada ya kuchelewa kuosha vyombo na kwamba licha ya kulia sana kutokana na kipigo alichompa, mama yake hakuridhika na kumuongezea adhabu kwa kumwagia maji ya moto kabla ya kumzoazoa na kumtupa kwenye shamba la mihogo. ’’Kule shambani nilikaa kwa masaa mengi nikilia...walimu nd’o wakawaita polisi na kuja kuniokoa,’’ akasema mtoto huyo wa darasa la pili ambaye anadai baadhi ya walimu walishuhudia namna alivyokuwa akichapwa na ndio maana alipokuwa haonekani wakapata wasiwasi na kuanza kumsaka kabla ya kumkuta kwenye mihogo akiwa hoi na kwenda kuripoti tukio hilo polisi. ’’Waliingiwa na wasiwasi na kuanza kunitafuta kwa sababu mama yangu wanamjua...ni mchapaji sana,’’ akasema mtoto huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa shida huku akibubujikwa machozi. Cha kusikitisha zaidi, binti huyo ambaye ana siku kadhaa sasa hospitalini Nyerere anasema: ’’Nasikia polisi ameshaachiwa kwa dhamana, lakini hajawahi hata kuja kunitazama hospitalini...aje tu anitazame, Mungu amenisaidia na sijafa kama alivyokuwa amepanga na kuniambia kuwa ananiua ili na yeye ajiue.’’ Kuhusiana na mahala pa kuishi baada ya kutoka hospitalini salama, binti huyo ambaye ana mabaka mengi yaliyotokana na maji ya moto aliyomwagiwa, akasema: ’’Sikubali kurudi nyumbani....bora niende kukaa kwingine kama kwa Mshashi Samson au kokote kule, naogopa mama ataniua kweli.’’ Akizungumzia hali ya bintyi huyo kufuatia sakata hilo ambalo mwandishi hakuweza kupata maelezo toka polisi, Mganga wa zamu hospitalini Nyerere, Donald Mwema, amesema kuwa hali ya bintyi huyo aliyekuwa hoi inaendelea vizuri akisema: ’’Namna alivyokuwa wakati akiletwa ni tofauti sana na sasa...anaendelea vizuri na kwakweli Mungu ni wa kumshukuru katika jambo hili la kusikitisha.’’ Baadhi ya walimu walio shule moja na mama mzazi wa binti huyo, wamemueleza mwandishi kuwa mwenzao (Mwl. Laurencia) ni mkali sana katika kuwaadhibu watoto na kwamba ndio maana waliamua kumsaka bintiye mara tu walipogundua kuwa amemchapa kupita kiasi. Alipofuatwa na mwandishi wa habari hii ili kuzungumzia sababu za kumsulubu bintiye kwa kiwango hicho cha kukaribia kumnyofoa roho, mama mzazi, Mwalimu Laurencia Shija aliyedai kuwa yuko ’fiti’ kiakili tofauti na baadhi ya watu walivyoanza kumvumisha, amekataa kuzungumza lolote kuhusiana na tukio hilo analodaiwa kulitenda kwa mikono yake na kuwaacha watu wakijiuliza maswali mengi bila majibu kuwa ni kwa nini akafanza mambo hayo kwa bintiye? Bila shaka dola iko kazini na itabainisha ukweli wa unyama huu dhidi ya mtoto Thecla Nyangige!

WAGONJWA WA KANSA
WAGONJWA WA KANSA
Niandikie